Skip to main content

NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII ATEMBELEA ENEO LITAKALOJENGWA STESHENI YA TRENI NA KITUO CHA HABARI KWA WATALII KATIKA PORI LA AKIBA SELOUS

Katika jitihada za kukuza pato la nchi kupitia utalii nchini, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi kupitia Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) ina mpango wa kujenga stesheni maalum ya treni na kituo cha habari watalii (Tourism Information Center) katika Pori la Akiba Selous -Kanda ya Kaskazini – Matambwe. Katika kufanikisha hilo, timu ya maandalizi ya mradi ikiongozwa na Dkt. Aloyce Nzuki ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ilitembelea eneo linalopendekezwa kwa ujenzi wa mradi huo tarehe 2/Jan/2018. Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kufanya tathmini ya eneo husika kwa kushirikisha wataalam wa pande zote mbili TAWA na TAZARA ili kufikia muafaka wa namna bora ya Kutekeleza mradi husika. 

Ikumbukwe mnamo mwezi Machi 2017 Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi kupitia Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) walianza mchakato wa kujadili pendekezo la upanuzi wa kituo kidogo cha treni Matambwe (Halt station) kuwa stesheni kamili.

Lengo Kuu;

(i)            Kutumia fursa ya reli ya TAZARA kuhudumia watalii kwa wingi zaidi tofauti na ilivyo hivi sasa,

(ii)            Kukuza utalii wa ndani kutokana na gharama ndogo ya usafiri wa treni ukilinganisha na njia nyingnine za usafiri,

(iii)           Kutumia fursa ya treni ya kitalii ya ‘Rovos’ kutoka Afrika ya Kusini kukuza utalii wa kimataifa kwa kuongeza safari zaidi,

(iv)          Kufungua fursa kwa TAZARA na wawekezaji wengine kuwekeza katika sekta ya utalii nchini,

(v)           Kuunganisha maneo mengine ya vivutio vya utalii katika Ukanda wa Kusini na Pori la Akiba Selous

Faida hizi zitaongeza thamani ya uwekezaji katika Pori la Akiba Selous ikiwemo sekta ya malazi pamoja na kufungua aina mpya ya package ya Utalii kwani Pori hili litakuwa ndio la kwanza kufikika kwa njia ya reli nchini na hivyo kuongeza mvuto kwa wageni ukilinganisha na maeneo mengine yenye vivutio vinavyofanana na Pori la Akiba Selous.

Aidha, mradi huu utaongeza chachu katika kufungua fursa mbalimbali za kichumi (economic multiplier effect) kwa wafanyabiashara mbalimbali katika sekta za migahawa, maduka ya zawadi (Curio shops) pamoja kuongeza fursa za biashara kwa wafanyabiashara wadogo wadogo pamoja na ajira kwa maeneo yanayo zunguka pori hili.

Katika mradi huu, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ndio mdau mkubwa wa mradi uliopendekezwa kwa kuwa Pori la Akiba la Selous lipo chini ya Mamlaka hiyo.

Ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huu, kuliainishwa maeneo mawili muhimu ambayo ni:

(i)             Ujenzi wa jengo la stesheni litakaloweza kutoa huduma za Kituo cha Habari kwa Watalii, sehemu ya kupumzikia kwa wasafiri wakati wa kuingia na kutoka kwenye treni, mgahawa, maduka ya zawadi (curio shops), maliwato (wash rooms) n.k.

 

(ii)           Utandazaji wa reli ya mchepuko kwa urefu unaotakiwa kuendana na mahitaji ya kituo ili kuruhusu treni za wageni wanaotembelea Pori la Akiba Selous kutoa huduma bila ya kuathiri matumizi ya treni nyingine zinazotumia njia kuu.

 

Kwa kuzingatia umuhimu wa Taasisi zenu na mchango mlionao katika nyaja wa kitaalamu na kifedha katika utekezaji wa mradi huu, nawakarbisha wote mlioshiriki ili tuweze kupata taarifa za mrejesho wa makubaliano ya vikao vilivyopita pamoja na kujadili kwa pamoja namna bora ya kufikia azma hii ya Serikali kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa letu.